SUMAYE AZIPONDA SIMBA NA YANGA


WAZIRI mkuu mstaafu Frederick Sumaye (pichani) ameeleza kusikitishwa kwake na kupoteza umaarufu wa soka la Tanzania kwa sasa ukilinganisha na miaka ya 1970.
Sumaye alisema hayo juzi katika hoteli ya Double Tree By Hilton ya jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwatunuku washindi mbalimbali waliofanya vema kwenye ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012.
Alisema hali hiyo inatokana na timu vilabu nguli vya Simba na Yanga kubweteka kwa moja kuifunga nyenzake na kujiona zimefika peponi kitu ambacho si dalili nzuri katika maendeleo ya soka.
“Simba kuifunga Yanga au Yanga kuifunga Simba si kigezo kizuri cha kujiona ni timu nzuri, timu inatakiwa iangalie ushindani kimataifa …ndiyo maana hata wakipangiwa timu kutoka Misri, Ivory Coast n.k mnaingiwa na hofu kubwa,”alisema.
“zamani vilabu vya nje vilikuwa vikipangwa na timu za Tanzania zinatetemeka lakini sisi sasa…kama tunataka kurudi katika heshima yetu ya zamani tujipange kimataifa, “aliongeza Sumaye.
Aidha, Sumaye alisikitishwa na migogoro katika vilabu na kusema inachangia pia kudidimiza soka hivyo amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano sambamba na kuvihudumia ipasavyo vilabu vyao.
Sumaye ambaye  ni mnazi mkubwa wa mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba, alitumia fursa hiyo kuwaasa mashabiki na wanachama wa timu za Simba na Yanga kuzomeana uwanja pindi moja ya timu inapokuwa uwanjani.
“Muwe wapinzani katika michezo lakini si uhasama, lazima tuwe na urafiki baina yetu na kuonyesha uzalendo zaidi kwa Simba kuishangilia Yanga ikicheza na timu ya nje au Yanga kuishangili Simba ikicheza na timu ya nje,”aliongeza.
Sumaye pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza washindi wote na kuwataka kutovimbishwa vichwa na zawadi hizo badala yake wazitumie kama kichocheo cha kujibiidiisha zaidi.