SIMBA SC YAPEWA VIFAA VYENYE THAMANI YA SH.MIL.18


KLABU ya soka ya Simba jana imepokea msaada wa jezi, raba, viatu vya kuchezea mpira, mabegi na suti za michezo (tracksuit) – vyote vya kisasa kabisa, kutoka kwa familia ya Al Ruwahi. Msaada huo umetolewa kwa mapenzi mema ambayo familia hiyo inayo kwa klabu. 
Ikumbukwe kwamba mahusiano baina ya familia ya Al Ruwahi (Ruwehi) na Simba yamedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Takribani miaka 30 iliyopita, familia hiihii ilitoa zawadi ya basi (Nissan Coaster) kwa Simba na kuifanya klabu yetu kuwa ya kwanza nchini kumiliki basi lake yenyewe. 
Msaada huo wa sasa kwa Simba una thamani ya Sh milioni 18 kwa ujumla wake na Simba sasa itavaa jezi hizo katika pambano lake la kesho dhidi ya Azam katika michuano ya Kombe la Kagame. 
Klabu ya soka ya Simba inatumia nafasi hii kuwakaribisha wapenzi na wanachama wake kujitokeza kuisaidia klabu kwa namna yoyote ile, kama ilivyofanya familia hii ya Al Ruwahi, ili kusukuma mbele gurudumu la  maendeleo ya klabu. 
Simba ni ya kila mmoja na haina mwenyewe. Umoja na mshikamano baina ya viongozi, wadhamini, wapenzi na wanachama wake, ndiyo utakaoifanya izidi kuwa bora hapa nchini na nje ya mipaka ya taifa letu.