SIMBA KUMKATIA RUFAA KATIBU MKUU WA TFF KUHUSIANA NA SUALA LA YONDAN


Simba Sports Club imesikitishwa na hatua ya Katibu Mkuu wa TFF kujichukulia mamlaka ya Kamati ya Katiba na Sheria na kuamua mustakabari wa suala la Kelvin Yondani kwa barua yenye kumb namba TFF/TECH/GC.12/62 ikijibu pingamizi la Simba Sports Club lililokuwa likitaka mgogoro huo uamuliwe na chombo husika.

Masikitiko hayo ya Simba Sports Club yanatokana na jinsi haki  na misingi bora ya uendeshaji wa mpira inavyoonekana kupindishwa waziwazi kwani Simba Sports Club imeshaandika barua nyingine mbili kwa Rais Tenga moja ya terehe 7/6/2012 yenye Kumb na SSC/5/6/02 ikilalamika juu ya uendeshwaji wa sakata zima la udanganyifu wa usajili wa mchezaji wa Simba Kelvin Yondani ambayo Rais alitoa maagizo kwa Katibu Mkuu na nakala kuja kwa Simba SC kwa barua pepe ya tarehe 8/6/2012 lakini baada ya kutofanyika utekelezaji wowote na badala yake watendaji wa TFF kuendelea kuongea katika vyombo vya habari wakisema mchezaji huyo ni mchezaji huru, Simba Sports Club iliandika barua nyingine kwa Rais Tenga juu ya kukosa imani na sekretarieti ya TFF  kwa barua ya tarehe 23/6/2012 yenye kumb na. SSC/24/6/02 jambo ambalo limeonekana wazi kwamba sekretarieti ya TFF haitendi haki kwa Simba kwa jinsi  ambavyo haikufanyia kazi barua mbili lakini Katibu Mkuu wa TFF amekuwa mwepesi wa kujibu pingamizi wakati si kazi yake ili mradi timu yake ya Yanga mabayo yeye ni mwanachama ifanikiwe jambo lake. 

Katika barua ya pingamizi dhidi ya mchezaji Kelvin Yondani kutumiwa na klabu ya Yanga katika michezo ya kirafiki na ile ya CECAFA  ya tarehe 11/7/2012 yenye kumb namba SSC/1/7/02 Simba Sports Club iliomba suala la mchezaji huyo lipelekwe katika kikao cha kamati ya katiba na sheria ambayo muda wake wa kukaa bado kwani kamati hiyo inaweza kukaa baada ya wiki mbili za kufunga usajili na kupokea pingamizi mbalimbali lakini taarifa za uhakika ni kwamba kamati hiyo ilijaribu kuitishwa haraka haraka ili kulitolea suala hili uamuzi lakini corum haikutimia hivyo ikashindwa kutoa maamuzi lakini kwa ubabe Katibu Mkuu akaamua kujichukulia mamlaka yasiyokuwa yake na kumpa leseni ya Yanga Kelvin Yondani huku Simba ikipokea majibu tarehe 14/7/2012 kwa barua uwanja wa Taifa wakati mechi kati ya Yanga na Atletico imeshaanza na ipo dakika ya 18.

Katika barua yake ya kumuidhinisha Kelvin Yondani katibu mkuu kakiri kuwepo kwa mkataba wa Yondani na Simba unaoisha mei 31, 2012 na kakiri pia kupokea nyaraka ya makubaliano ya Simba SC na Kelvin Yondani lakini kwa sababu yeye si mwanasheria na ndio maana kazi hiyo ni ya kamati ya katiba na sheria amezitafsilia pande mbili za mkataba yaani Simba Sports Club na Kelvin Yondani nia yao wakati wanaingia mkataba kwamba mkataba utaanza tarehe 23 december 2012 na kuweka kiambatanisho cha sehemu ya kusaini ya Simba Sports Club ambayo kwa sababu za kibinadamu ilikosewa na inasomeka tarehe 23 december 2012.

Katibu Mkuu wa TFF ameshindwa/amejikataza kuusoma mkataba tangu mwanzo na kuona nia za pande za mkataba ni zipi kwani katika ukurasa wa kwanza mkataba unasoma kwamba umesainiwa tarehe 23/12/2011, pia mkataba unatambua uwepo wa mkataba wa pande hizo mbili unaoisha tarehe 31/5/2012 na pande husika katika mkataba zimeonyesha nia ya kuongeza mkataba mara tu ule wa awali unapoisha.

Katika kipengele cha kwanza mkataba umeshuhudia pande zikitamka waziwazi kwamba mkataba umeongezwa kuanzia (effective) tarehe 1/6/2012 mara tu mkataba wa awali unapoisha sasa inashangaza Katibu Mkuu anazitafsilia pande nia zao kwamba mkataba utaanza tarehe 23/12/2012 wakati mkataba umetamka waziwazi.

Pia sehemu aliposaini mchezaji Kelvin Yondani imeonyeshwa waziwazi kwamba kasaini tarehe 23/12/2011 hivyo kuacha hitimisho lisilo na shaka kwamba Katibu Mkuu wa TFF amekiuka na kujivika mamlaka yasiyo yake ili kutekeleza unazi wake wa Yanga.

Simba Sports Club inakusudia kuyakatia rufaa maamuzi haya ya Katibu Mkuu wa TFF na ipo  tayari kufuata mikondo yote ya sheria mpaka haki ipatikane kwani itatumia taasisi za TFF kwanza na isiporidhishwa na maamuzi itapeleka suala hili CAF mpaka FIFA na jambo la kushukuru ni kwamba Shirikisho la TFF limeanza kujibu barua za Simba SC suala ambalo linaanza kutoa mwanga wa nia ya kutotenda haki lakini barua hizo zitasaidia kuwaonyesha watu wa nje kama tukifika huko jinsi mpira wa Tanzania unavyoendeshwa kinazi na viongozi wa Shirikisho.

Imetolewa na 
Simba Sports Club

Comments