SIMBA, AZAM ZANG'ARA KOMBE LA URAFIKI


Shujaa wa Simba SC leo, Felix Sunzu

Na Prince Akbar,
BAO pekee la mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya 58, usiku huu limetosha kuipeleka Simba SC Nusu Fainali ya Kombe la Urafiki, baada ya kuilaza timu ya taifa ya vijana ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 23, Karume Boys kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika mchezo wa wali, Azam ilifanikiwa kutinga Nusu Fainali baada ya kuifunga Mafunzo, mabao 3-2.
Mabao ya Azam yalifungwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya sita, baada ya kupiga kona iliyotinga moja kwa moja nyavuni, kabla ya Kipre Tcheche kuunganishia nyavuni krosi ya Abdulhalim Humud ‘Gacuho’ dakika ya 37 na Ibrahim Mwaipopo kupiga la tatu dakika ya 83.
Mafunzo, ambayo imepangwa kundi moja na Azam katika Kombe la Kagame, michuano inayotarajiwa kuanza wiki ijayo, mabao yake yalifungwa na Mohamed Abdulrahman dakika ya 46 na Jaku Joma dakika ya 62.
Smba imemaliza kama kinara wa Kundi A, kwa pointi zake saba, ikishinda mechi mbili na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi tano, baada ya kushinda mechi hiyo moja tu na kutoa sare zote dhidi ya U23 ya Zanzibar, maarufu kama Karume Boys na Simba SC, wakati Mafunzo imeaga bila ya kuokota hata pointi moja, baada ya kufungwa mechi zote na Azam, Karume Boys na Simba. Karume imemaliza na pointi nne na imetolewa.
 
SOURCE: BIN ZUBEIRY (http/bongostaz.blogspot.com)