SERIKALI YAENDELEA NA MPANGO WA KUWAANDAA MAKOCHA WAZAWA

Na Lydia Churi, MAELEZO-Dodoma 
Serikali inaendelea na mkakati wa kuwaandaa makocha wazawa ili waweze kutambulika na kutumika kufundisha timu za hapa nchini kama yalivyo matarajio ya watanzania wengi.
Akijibu swali Bungeni mjini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Amos Makalla alisema serikali inatambua umuhimu wa makocha wazalendo katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Alisema makocha wazawa ndiyo wanaotumika kufundisha timu za hapa nchini kuanzia ngazi za Vijiji, Wilaya, Mikoa na hata baadhi ya timu za Taifa. Aliongeza kuwa Tanzania ina makocha wazawa tisa wenye uwezo wa kimataifa.
“Makocha wa kigeni ni wachache na si kwa michezo yote, hivyo mkakati wa serikali ni kuhakikisha inawaandaa makocha wazawa wengi zaidi ili watumike na hatimaye kupunguza gharama za kuajiri makocha wa kigeni,”alisema.
Naibu Waziri huyo alisema hata hivyo ni utaratibu wa kawaida katika sekta ya michezo duniani kote kuwa na makocha wa kigeni katika baadhi ya michezo ambao wameonekana kukubalika na kuaminika zaidi kwa wachezaji.
Alisema, kwa kutumia makocha wa kigeni, makocha wazawa wamekuwa wakifaidika na mafunzo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiendeshwa na makocha hao wa kigeni. Makocha wa kigeni wengi wamekuwa wakifundisha kwa kusaidiwa na makocha wazawa ambao hufaidika kwa kujifunza mbinu mbalimbali za ufundishaji kwa kuambatana nao.
Alisema, kwa kutumia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, mafunzo mbalimbali ya ualimu na uamuzi kwa makocha wazalendo hutolewa ili kuwaongezea ujuzi katika fani.
Alisema, serikali kwa kutambua umuhimu wa michezo kuanzia ngazi ya chini iliamua kurejesha mashindano ya michezo ngazi ya shule za msingi (UMISHUMTA) na ngazi ya shule za sekondari (UMISETA) ili kuwajengea uwezo wa kimichezo wanafunzi hao.
Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Dimani, Mheshimiwa Abdalah Sharia Ameir aliyetaka kujua kwa nini serikali inatumia fedha nyingi kuajiri makocha wa kigeni wakati nchini wapo makocha wazawa wengi wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Comments