MWANZA YAING’OA KINONDONI COPA COCA-COLA 2012


Mwanza imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo (Julai 11 mwaka huu) kuitoa Kinondoni kwa penalti 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. 
Hadi dakika 90 za mechi hiyo ya robo fainali zinamalizika timu hizo zilikuwa hazijafunga, hivyo kulazimika kuingia kwenye mikwaju ya penalti ili kupata mshindi ambaye atacheza nusu fainali keshokutwa (Julai 13 mwaka huu) dhidi ya Temeke. 
Walioifungia Mwanza katika penalti ni Christopher Maghinwa, Steven Lubela na Juma Masunga. Penalti ya Kinondoni ilitiwa wavuni na Shabani Nyenje. Waliokosa kwa Kinondoni ni Miza Abdallah, John Komba na Juma Masunga. 
Nusu fainali ya pili itakuwa kati ya Morogoro na mshindi wa mechi ya robo fainali kati ya Dodoma na Tanga itakayochezwa leo jioni (Julai 11 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo.