MWANDISHI TANZANIA DAIMA AULA COREFA


KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), imemteua mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima na Radio Clouds FM, Victor Masangu, kuwa msemaji mpya wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa uteuzi huo, Katibu Mkuu wa COREFA, Riziki Majala, alisema kwamba kamati imeamua kumteua Masangu, kutokana na mchango wake na uwezo alionao katika kuleta maendeleo ya mchezo wa soka ndani ya Mkoa wa Pwani.
 “Sisi kama kamati ya utendaji, katika kuhakikisha kwamba masuala mbalimbali ambayo tutakayokuwa tukiyajadili yanafikishwa kwa jamii nzima, hasa wapenzi wa mchezo wa kandandana, ndiyo maana tukaamua kumteua Masangu awe ndiye msemaji wa chama,” alisema Majala.
Majala aliongeza kuwa, pamoja na uteuzi huo, Masangu ndiye atakayekuwa Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya habari na uenezi, ambapo Makamu wake ni Ben Komba, huku wajumbe ni Alex Luambano na Shafii Dauda.
Katibu huyo alifafanua kuwa, msemaji wa zamani, Masau Bwire, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya COREFA, makamu wake ni Mathew Shayo na wajumbe ni Mohamed Amiri, Haji Manara na Nicholous Makini.
Kwa upande wa Kamati ya Nidhamu, Mwenyekiti ni Shujaa Sachore, Makamu Peter Hokororo na wajumbe ni Ally Abdalah, Musa Athumani na Mustapha Julius.