MILOVAN KUREJEA KESHO TAYARI KUIPA MAKALI SIMBA SC


WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wakianza mazoezi jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Milovan Circovick anatarajiwa kurejea nchini kesho.
Milovan anarejea kutoka kwao Serbia alikokwenda kwa mapumziko mafupi baada ya timu yake ya Simba kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Kagame wiki iliyopita katika hatua ya robo fainali.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, baada ya kurejea, Milovan ataanza kuisuka timu yake kwa Tamasha la ‘Simba Day’ litakalofanyika Agosti 8.
“Ni matarajio yetu kocha atarejea hiyo Jumatano kama ilivyopangwa ili aweze kuendelea na programu yake ya kukinoa kikosi,” alisema.
Alisema, wachezaji wote wa Simba jana asubuhi walianza mazoezi ufukweni kabla ya jioni kuhamia viwanja vya TCC, Chang’ombe.
Aidha, Kamwaga alisema maandalizi ya mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Agosti 5 kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oyesterbay yanakwenda vema.
Alisema kila mwanachama anayetaka kushiriki  mkutano huo anapaswa kuwa hai, hivyo alipie kadi kuepuka usumbufu siku ya mkutano.