MGOMBEA UENYEKITI YANGA AMWANGA SERA ZAKE

 Sports Lady Dina Ismail akizungumza na mgombea uenyekiti wa Yanga, Edger Chibura


MGOMBEA nafasi ya uenyekiti katika klabu ya Yanga, Edgar Chibura amepania kuondoa utegemezi ndani ya klabu hiyo iwapo atafanikiwa kutwaa nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai 15 katika ukumbi wa Diamond Jubillee jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza jijini Dar es Salaam , Chibura alisema kwamba Yanga ni klabu kubwa hivyo ni muhimu kujitegemea yenyewe kwa kuwa na vyanzo muhimu vya mapato badala ya kutegemea wafadhili zaidi. 
Alisema mbali na hilo, iwapo atachaguliwa kuingoza Yanga katika kipindi chake cha uongozi ataleta umoja na mshikamano ndani ya klabu hiyo sambamba na kuweka uwazi wa mapato na matumizi kwa wanachama. 

 Chibura akizungumza na Sports Lady Dina Ismail


Chibura ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliongeza kuwa iwapo atachaguliwa kuongoza Yanga, atasimamia mabadiliko ya Katiba ya Yanga kwa kuwashirikisha viongozi wa matawi yote ya Yanga nchini ambao watawasilisha mapendekezo ya wanachama. 
Aidha, Chibura aliongeza kuwa kupitia uongozi wake, ataboresha kitengo cha habari kwa kuongeza maofisa, kuanzishwa kwa kituo cha televisheni cha Yanga, kuanzishwa kituo cha redio na pia kituo maalum cha utalii am,bacho kitakuwa kinahusisha masuala ya klabu hiyo tu. 
“Pia ndani ya uongozi wangu nitahakikisha Yanga inakuwa na Uwanja wake wa kisasa mbali na huo wa Kaunda…tutashirikiana na bviongozi wenzangu kutafuta eneo ambalo huko tutajenga uwanja mkubwa, utakaokuwa na vitega uchumi kadhaa, pamoja na hosteli,”aliongeza. 



Kwa wasiomfahamu Chibura, aliwahi kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Makongo tangu mwaka 2001 hadi 2010 kabla ya kuhamia wizara ya Elimu anapotumikia hadi sasa, pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Abajalo ambapo aliiiwezesha kutoka daraja la tatu hadi la kwanza, huku ikipitiwa na nyota kama Ali Mayay, Aron Nyanda, Lucas Matokeo, Kalimangonga Ongala na wengineo. 
Katika uchaguzi huo, Chibura ambaye atazindua kampeni zake kesho mkoani Morogoro,atachuana na mfanyabiashara na aliyepata kuwa mfadhili wa klabu hiyo Yusu Mahboob Manji, pamoja na mdau mkubwa wa michezo nchini, John Jambele.

Comments