MADINA UNASHUPALIA USAGAJI, LIGI NAYO VIPI?


Na Ruhazi Ruhazi
NINAAMINI nguvu iliyotumiwa na Mwenyekiti wa Chama cha soka la wanawake (TWFA) Madina Kessy na viongozi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kwa upande mwingine kujaribu kuzima kashfa ya usagaji iliyoikumba timu ya soka ya wanawake ‘Twiga Stars’ ingetumika kwa ajili ya maendeleo ya soka la wanawake, tungekuwa mbali.
Twiga Stars timu inayookoteza wachezaji wa kuichezea baada ya TWFA na TFF kushindwa kuendesha Ligi soka ya taifa ya wanawake, iling’olewa na Ethiopia katika mechi za mwisho za kusaka tiketi ya fainali za Afrika zitakazofanyika Novemba, Mwaka huu Guinea ya Ikweta.
Timu hiyo ilikosa tiketi hiyo kwa kufungwa mabao 2-1 ugenini Adis Ababa, Ethiopia na viongozi wa timu hiyo akiwemo aliyekuwa Kocha Mkuu wake Charles Boniface Mkwasa wakaja na utetezi kwamba kilichowaangusha ni hali ya hewa na hujuma waliyofanyiwa na wapinzani wao.
Hata hivyo, utetezi wao ulikuwa dhaifu kwani wakicheza mechi ya marudiano mbele ya maelfu ya Watanzania kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, waligungwa tena
bao 1-0, hivyo safari ya Guinea ya Ikweta, ikaishia hapo.
Baada ya hapo, harakati za kumsaka mchawi zikaanza kwa kuibuliwa suala la wachezaji
wa timu hiyo kukosa maadili ya kisoka, likiwemo suala la kusagana, hivyo kuathiri ufanisi
wa timu hiyo dimbani.
Hili likawachoma na kuwaumiza mno viongozi wa TWFA akiwemo Madina na Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis wakiamua kuitisha mkutano kwenye ofisi za TFF.
Lakini, ili kupata utetezi wa haja juu ya jambo hilo, waliamua kumjumuisha mpaka aliyekuwa kocha wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa, licha ya kwamba alishajiuzulu kuinoa timu hiyo kutokana na matokeo mabaya.
Nilistaajabu kuona viongozi hao wakionekana kuguswa na kuhamanika kwa madai hayo ya kashfa lakini sivyo wanavyoguswa na kukosekana kwa Ligi soka ya wanawake nchini.
Ni hapo ambapo kila mdau wa soka atahisi na kuziamini hisia zake kwamba kinachowafanya viongozi hawa kutikisika kwa kashfa ndogo kama hiyo ni kutokana na kuhisi kuwa maslahi yao yataharibika, lakini wakisahau kuwa kutosimama kidete kuhakikisha kuwa soka la wanawake nchini linapiga hatua tayari ni dosari inayotishia ulaji wao.
Kibaya ni kwamba sio Madina, Furaha wala Kocha aliyeeleza namna walivyofanya uchunguzi wao ili kujiridhisha kuwa kashfa hizo hazipo kwa wachezaji wao, zaidi ya kusema mwenye ushahidi ajitokeze na kuwathibitishia.
Nilitamani kucheka kwa sababu sote twafahamu kuwa waandishi waliandika kile walichoelezwa kwa hiyo ilikuwa juu yao kufanyia uchunguzi kabla ya kutaka kujisafisha kwani masuala hayo hufanyika kwa siri hivyo wao walipaswa kufanya uchunguzi wa siri pia, sio kutka tu kujisafisha eti kwa hofu kuwa wazazi wataanza kuwazuia watoto wao wa kike kujifunza na kucheza soka.
Ni wazi kuwa, kashfa hizi za usagaji zisingeibuliwa kama Twiga Stars ingeishinda Ethiopia na kutinga fainali za Afrika kwa wanawake.
Tangu  tulipoanza kukutana na Ethiopia katika fainali za kuwania kufuzu kwa mashindano mbali mbali ya soka kwa wanawake mwaka 2002, hatujawahi kushindwa hata mchezo mmoja.
Nakumbuka kuwa Ethiopia waliwahi kuambulia sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam
(Uhuru) mwaka huo wa 2002, lakini sisi tukasonga kwa sababu tuliwafunga mabao 3-2 nyumbani kwao.
Lakini, katika kuonesha kuwa hakuna kinachofanywa kukuza soka la wanawake nchini, safari hii Ethiopia imetufunga katika michezo yote miwili.
Hata hivyo, kiashirio cha kushuka kwa kiwango cha soka letu kilionekana pale tulipokubali kuwa gunia la mazoezi la
timu za Zimbabwe na Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ambazo zilitufunga idadi kubwa ya mabao kwwenye uwanja wa taifa tulipocheza nazo mechi za kirafiki wakati tukijiandaa kucheza na Ethiopia.
Nakumbuka siku akina Madina na wenzake wakihangaika kujisafisha na kashfa ya usagaji pale TFF, nilimuuliza haoni haja ya kujiuzulu kwa kushindwa kulisaidia soka la wanawake lipige hatua kiasi kwamba ameshindwa hata kuasisi michuano maalum itakayohusisha Mikoa yote nchini kama ameshindwa kuendesha Ligi soka ya wanawake, majibu yake yakawa “Siwezi Kujiuzulu”.
Hata hivyo, nilimtafakari jinsi Madina anavyotaka asafishwe kiasi cha kufikia hatua ya kuomba kukutana na vyombo vya habari ili tu aondokane na kashfa hiyo ya usagaji inayosemwa kila kona ya nchi hivi sasa ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha kuvuja kwa siri hiyo ni baadhi ya wachezaji wenyewe wa Twiga, ambao wamesema kuwa wapo wenzao waliokubuhu kwa mchezo huo ndio maana viwango vyao vimeshuka.
Ni hapo hoja ya umuhimu wa kuwepo kwa Ligi soka ya wanawake inapokuwa na mashiko, lakini kwa bahati mbaya sana Madina na wenzake wa TFF hawalioni hilo, zaidi ya kubaki wakijinasibu kwamba hupokea mgao maalum kutoka Shirikisho
la soka la Kimataifa (FIFA) kwa maendeleo ya soka la wanawake.
Kwa sababu kuwepo kwa Ligi kutapanua uwigo wa kocha wa Twiga Stars kuchagua wachezaji bora na wasio na kashfa,  tofauti na sasa ambapo vyovyote atakavyofanya.
Sijui watu hawa watatuambia maendeleo hayo ya soka la wanawake yanayopigiwa upatu hata na FIFA ni yepi zaidi ya kuwa na Ligi bora pamoja vituo vya kuibua na kuendeleza soka la wanawake?.
Nadhani hii kashfa inayowaliza kwa baadhi ya wachezaji wao kuhusishwa na masuala ya usagaji ni ndogo kama timu itaendelea kufanya vibaya, huenda tukajionea au kusikia kashfa nyingine nzito zaidi ya hizo na ambazo pengine zikawaweka pabaya zaidi viongozi hao, TFF na mustakabali wa soka la wanawake kwa ujumla.
       

Comments