KOMBE LA KAGAME LAGEUKA DILI JANGWANI


KOMBE la ubingwa wa Afrika Mashariki  na Kati maarufu kama Kombe la  Kagame jana liligeuka kuwa dili baada ya mashabiki wa klabu hiyo kutozwa sh 2,000 ili kupiga nalo picha.
Yanga ilitwaa ubingwa huo wa pili mfululizo Jumamosi iliyopita baada ya kuitandika Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na furaha za ubingwa huo baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimiminika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Jangwani na Twiga kwa lengo la kupiga picha ya kumbukumbu na kombe hilo.

Hata hivyo mashabiki hao wamejikuta wakitozwa kiasi hicho cha fedha na mtu anayeendesha zoezi la upigaji picha hizo.
“Ni kweli mashabiki wanatozwa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kupiga picha na kombe,” alisema Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Tom Saintfiet amewapa mapumziko ya siku nne wachezaji wa timu hiyo mara baada ya kazi ngumu ya kushiriki michuano ya Kagame na kufanikiwa kulibakisha kombe Jangwani.
Saintfiet alisema kutokana na hatua hiyo wachezaji hao hawana budi kupata mapumziko ya siku hizo na hatimaye Ijumaa wataanza rasmi maandalizi yao ya Ligi Kuu Bara.

Comments