CLEMENT SANGA:ANAYEWANIA M/MWENYEKITI YANGA MWENYE MPANGO WA KUIJENGA YANGA KIUCHUMI


Sanga, amewasihi wanachama wa klabu hiyo kumpatia kura katika uchaguzi huo ilii aweze kushirikiana na wengine kuijenga Yanga imara kisoka na kiuchumi.
Anasema  kama atapewa ridhaa ya kuingia madarakani, atajitahidi kupigania umoja miongoni mwa viongozi na wanachama.
Alisema licha ya kila mwanachama kutaka mafanikio ya soka na kiuchumi, lakini mshikamano ndio nyenzo muhimu ya kufikiwa kwa mafanikio hayo.
Mgombea huyo alisema ataimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama kuanzia kwa vijana hadi wazee bila kuvisahau vikundi vya uhamasishaji ambavyo licha ya kufanya kazi kubwa, vimekuwa havipewi heshima yake.
Sanga anabainisha kwamba kingine, atakachopigania kwa kushirikiana na viongozi wengine kama atashinda, ni uwekezaji kwenye soka ya vijana kwani huo ndio msingi wa mafanikio ya soka kote duniani.
Kuhusu uchumi wa klabu, ni kuhakikisha Yanga inakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato kama uwanja na jina lake kutumika kibishara zaidi tofauti na ilivyo sasa.
Aidha, atajitahidi kuwawezesha wanachama kiuchumi kwa kuanzisha Mfuko wa Akiba na Mikopo kwa Wanachama (Saccos) ambao utakuwa ukitoa mikopo kupitia matawi yao. 
Juu ya uendeshaji wa klabu, Sanga alisema akishinda, ataunda Idara za Uhasibu, Masoko, Sheria  na Habari, Mawasiliano na Uhusiano kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi.
Sanga alisema, jambo jingine ni  uimarishaji wa matawi ya klabu hiyo ikiwemo kuwaelimisha wanachama umuhimu wa kuichangia klabu yao.
Alisema, kuwepo kwa msingi imara kisoka na Kiuchumi, Yanga itaweza kuwa na kikosi imara Dimbani, hivyo kufanya vema kwenye michuanoya kitaifa na kimataifa.
Hata hivyo, akasisitiza suala la uvumilivu wa wanachama dhidi ya uongozi kwani mafanikio hujenga kupitia mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.  
Sanga alisema kama akipata ridhaa ya kuingia madarakani, atashirikiana na wenzake kuangalia pia uwezekano wa kufanyia marekebisho katiba ili iweze kuendana na wakati.
Kwa mazingira hayo, Sanga amewasihi wanachama wa klabu hiyo kuutumia vizuri muda wao wa kutoka nyumbani hadi ukumbini kwa kumchagua yeye na wengine kwa ajili ya maendeleo ya klabu hiyo kisoka na kiuchumi.

Comments