BIN KLEB:ALIYEPANIA KUIFIKISHA YANGA NANE BORA AFRIKA


WANACHAMA wa Yanga ni nani asiyemfahamu Binkleb kutokana na michango ya kuinusururu klabu hiyo pindi ilipotetereka, ikiwemo kugharamia kambi ya wachezaji baada ya viongozi kujivua gamba.
Kama hiyo haitoshi Binkleb ndiye aliyemsajili kiungo wa kimataifa wa Rwanda Haruna Niyonzima, pia kwa kushirikiana na swahiba wake Seif Ahmed ‘Magari’ wamemleta kocha wa sasa, Mbelgiji Tom Saintfiet na mengineyo.
Bin Kleb anasema ameamua kujitosa kuwania Yanga ili kuendeleza mpango wake wa kuisaidia Yanga ili iweze kupata mafanikio ikiwemo kushiriki hatua ya nane bora ya michuano ya Afrika.
“Ninataka ndani ya miaka miwili Yanga iwe katika matawi ya juu katika bara la Afrika na hilo litaambatana na usajili mzuri na uwekezaji katika timu za vijana na makocha waliobobea,” anaongeza.
Mbali na hilo, mgombea huyo anasema iwapo atafanikiwa kutwaa nafasi hiyo, kwa kushirikiana na viongozi wenzake atahakikisha kunakuwepo na uwazi wa mapato na matumizi kwa wanachama kila baada ya miezi mitatu.
“Pia nitasaidiana na wenzangu kuleta mfumo wa kuendesha miradi endelevu kwa manufaa ya klabu ili iondokane na mfumo wa sasa wa utegemezi,” anaongeza.
Aidha Bin Kleb anasema iwapo atapata fursa ya kuongoza Yanga pia atashirikina na viongozi wenzake kutengeneza miundombinu ikiwemo kuweka nyasi bandia katika Uwanja wa Kaunda hali ambayo itaziwezesha timu zao kufanya mazoezi kikamilifu.
“Nachukua fursa hii kuwaomba wanachama wa Yanga kunichagua ili niendeleze mambo mazuri,” anaongeza.

Comments