AUNT EZEKIEL APONDA WANAOTUMIA MKOROGO


MWIGIZAJI, mtayarishaji mahiri wa filamu nchini na balozi wa Zuku Swahili Movie, Aunt Ezekiel, amesema kuwa ataendelea kuilinda rangi ya ngozi yake kwa kutotumia vipodozi vikali ‘mkorogo’ ili kuwa mweupe.
Akizungumza hivi karibuni, msanii huyo alisema kuwa, anachokifanya yeye ni kujua aina ya vipodozi anavyostahili kutumia, lakini si vile vya kumbadili, ikiwamo rangi ya ngozi yake.
Msanii huyo, aliyasema hayo wakati akizungumzia juu ya kuteuliwa kwake pamoja na Jacob Stephen ‘JB’ kuwa mabalozi wa king’amuzi cha Zuku kwa upande wa wasanii, inayojulikana kwa jina la Zuku Swahili movie.
“Kwa kweli ninashukuru kwamba, sijawahi wala sitarajii kutumia mkorogo ili niwe mweupe, ninaridhika na ngozi yangu na naamini ndiyo inayonifanya niwe kipenzi cha wengi na ningewaomba wasichana kote nchini, ambao hawajatumia wasithubutu, kwani kuna madhara makubwa,” alisema.
Msanii huyo alisema kuwa, anaamini Zuku Swahili Movie, itawasaidia kukuza soko la kazi zao, kwa kuwa itakuwa ikionesha zaidi filamu nyingi za Kitanzania, kutoka Swahiliwood pamoja na tamthilia, vichekesho, kwaya na kazi zingine za sanaa zinazotumia Lugha ya Kiswahili kutoka nchi za Afrika Mashariki.