3,000 TU KUZIONA NGORONGORO HEROES, FLYNG EAGLES J'2


Hatimaye timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria (Flying Eagles) imewasili nchini leo mchana (Julai 26 mwaka huu) kwa ndege ya RwandAir ikiwa na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji 18. 
Awali timu hiyo ilikuwa iwasili jana jioni (Julai 25 mwaka huu) ikitokea Kigali, Rwanda lakini ikashindwa baada ya kuchelewa ndege. Flying Eagles itapambana na Ngorongoro Heroes katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Jumapili (Julai 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. 
Mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani nchini Algeria itachezeshwa na waamuzi kutoka Kenya wakati Kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda. 
Flying Eagles ambayo iko chini ya kocha John Obuh, Julai 24 mwaka huu ilicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali na kufungwa bao 1-0. 
Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris Green umefikia hoteli ya Rungwe iliyoko Mtaa wa Livingstone, maeneo ya Kariakoo.
Baadhi ya wachezaji walioko katika kikosi cha Flying Eagles ni Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar, Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune, Hassan Abubakar na Yahya Adamu. 
Makocha wote, Jakob Michelsen wa Ngorongoro Heroes na Obuh wa Flying Eagles wakiwa na manahodha wao, Jumamosi (Julai 28 mwaka huu) saa 4 asubuhi watazungumza na waandishi wa habari juu ya walivyoviandaa vikosi vyao kwa ajili ya mechi hiyo. Mkutano huo utafanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). 
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

Comments