14 ZATINGA 16 BORA COPA COCA-COLA 2012


Wakati 16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inaanza Jumamosi (Julai 7 mwaka huu) timu 14 zitakazocheza hatua hiyo zimeshajulikana baada ya mechi zilizochezwa leo (Julai 5 mwaka huu) katika viwanja vinne tofauti. 
Tanga iliyoigaragaza Kaskazini Pemba mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam imechukua moja kati ya nafasi nne kutoka kundi B. Mabao ya Tanga yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 30, 55 (penalti) na 58 wakati lingine lilifungwa dakika ya 53 na Issa Mwanga. 
Kwa ushindi huo, Tanga iliyofikisha pointi tisa inaungana na Mjini Magharibi yenye pointi 13, Morogoro pointi 12 na Mwanza pointi 11 kutoka kundi hilo kucheza hatua ya 16 bora. 
Mara iliyoichapa Mtwara mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam na kufikisha pointi tisa nayo imepata tiketi ya 16 bora kutoka kundi C ikiungana na Dodoma yenye pointi 12, Kinondoni pointi 11 na Temeke pointi tisa. 
Mabao ya Mara ambayo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa 3-0 yalifungwa na George William dakika ya pili, Edson Mwara dakika ya 17 na 45, na Hassan Ally dakika ya 88. Mtwara walipangusa machozi dakika ya 36 kwa bao la Ramadhan Njunja. 
Ndoto za Ilala kucheza 16 bora zimeyeyuka baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya vinara wa kundi A Ruvuma kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mbali ya Ruvuma iliyofikisha pointi 16, timu nyingine zilizopata tiketi ya 16 bora kutoka kundi hilo ni mabingwa watetezi Kigoma wenye pointi 12, Rukwa pointi kumi na Arusha pointi nane. 
Mchuano wa kupata timu mbili za mwisho kucheza 16 bora uko katika kundi D ambalo linasubiri matokeo ya mechi ya leo jioni kati ya Kusini Unguja na Tabora itakayochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.
 Kagera ambayo leo imeifunga Shinyanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu ni moja kati ya mbili ambazo zimeingia 16 bora kutoka kundi hilo. Nyingine ni Kilimanjaro iliyoongoza kwa kufikisha pointi 18 ikifuatiwa na Kagera yenye pointi tisa. 
Nafasi mbili zilizobaki zinawaniwa na Pwani yenye pointi saba, Singida (7), Tabora (6) na Kusini Unguja yenye pointi nne.

Comments