ZANZIBAR HEROES YATINGA NUSU FAINALI WORLD CUP


TIMU ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, imefanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizo wanachama wa Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa), inayoendelea nchini Kurdistan.
Baada ya Heroes kuanza kwa kishindo michuano hiyo kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Latia, juzi usiku walivuna ushindi wa
pili wa mabao 3-0 dhidi ya Tamil Elaam kwenye uwanja wa Erbir.
Kwa ushindi huo, Heroes chini ya Kocha Mkuu wake Hemed Moroko, wamemaliza vinara katika kundi lao la B, lililokuwa na timu tatu, ikiwemo Ratia.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Chama cha soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zacharia, Heroes wamekuwa gumzo kwenye michuano hiyo maarufu kwa jina la Viva World Cup.
Heroes walianza kupata bao la kwanza dakika ya 22, likifungwa na Khamis Mcha, ambalo lilidumu hadi timu
hizo zinakwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa kizuri kwa Heroes, kwani dakika ya 61, walifunga bao la pili likipachikwa wavuni na Amir Hanad kabla ya Awadh Juma kufunga la tatu dakika ya 90.
Katika hatua ya nusu fainali, Heroes leo itacheza na Cyprus iliyotoka kundi C, ambayo ilisonga mbele licha ya kufunga mabao 2-1 na Province ya Ufaransa.
Mechi nyingine ya nusu fainali, itawakutanisha wenyeji wa michuano hiyo Kurdistan dhidi ya Province, itakayochezwa leo usiku huku fainali ikichezwa kesho.
Kocha Moroko wa Zanzibar Heroes, amesema kikosi chake kipi fiti kukabiliana na ushindani wa leo, akitaka kutinga fainali na ikiwezekana kurejea na ubingwa.
Heroes wamekwenda huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, akiahidi shilingi mil 18 kama wakitwaa ubingwa na nusu yake, wakinusa fainali.