USAJILI WA DAN MRWANDA SIMBA WAZUA MINONG'ONO


USAJILI wa Danny Mrwanda katika klabu bingwa ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2011/2012  Simba,  umezua jambo baada ya kamati ya ufundi ya klabu hiyo kutokubaliana nao. 
Awali nyota huyo aliyewahi kukipiga Simba kabla ya kutimkia katika klabu ya DT Long An ya Vietnam, aliomba kusajiliwa tena Simba kwa masharti maalum lakini kamati ya ufundi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake Ibrahim Masoud ‘Maestro’ ilipinga. 
Habari kutoka Simba zinaeleza kuwa Mrwanda alitaka asajiliwe kwa dau la shilingi milioni 12  huku pia mkataba wake umruhusu kwenda katika timu yoyote atakayoipata nje ya nchi,kitu ambacho kilipingwa na kamati ya ufundi. 
Hata hivyo pamoja na kamati ya ufundi ya Simba kupinga usajili wa mchezaji huyo, makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliamua kumsainisha mkataba mshambuliaji huyo. 
Mmoja ya viongozi wa Simba ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini alisema wanasikitishwa na kitendo kinachofanywa na Kaburu kwani kamati ya ufundi ndiyo inajua ubora au udhaifu wa mchezaji sambamba na mapungufu yaliyopo ndani ya timu. 
Alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na matokeo yake wengi wa wachezaji ambao wamekuwa wakisajiliwa ‘kimabavu’ wameshindwa kutoa mchango wowote ndani ya timu hiyo. 
“Ndiyo tunajua Kaburu ana nguvu na uwezo mkubwa katika timu lakini kwa nini aingilie kazi za kamati ya ufundi,kama ni hivyo hakukuwa na maana ya kuwepo kwa hiyo kamati,”alisema mtoa habari huyo.