TUMEKUFA KIUME-KOCHA STARS


KOCHA wa Tanzania, Kim Poulsen amesema baada ya kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji sasa atajipanga upya kwa ajili ya mashindano yajayo kwani timu yake imeonyesha uwezo mkubwa katika mechi hiyo ya Jumapili. 
Kim alishudia Taifa Stars, ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiondolewa na Msumbiji kwa penalti 6-7 baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare 1-1 kwenye mchezo huo wa kusaka kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2013. 
Akizungumza na vyombo vya habari Kim alisema  Stars walicheza vizuri  lakini Mozambique walitumia nafasi nzuri ya kuwa nyumbani na kushinda. 
"Nawapongeza kwa kushinda, lakini najivunia vijana wangu kwa jinsi walivyoweza kucheza kwa umakini muda wote wa mchezo huu. 
"Nilijua Msumbiji wangeshambulia kwa nguvu,lakini na sisi tuliweza kucheza soka yetu ya kawaida na kutegeneza nafasi nyingi nashukuru tumeweza kusawazisha katika penalti lolote linaweza kutokea. 
Naye kocha wa Msumbiji,Gert Engels aliwasifu Stars kwa kucheza vizuri, huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo huo. 
"Tanzania ni timu nzuri inacheza kwa uwelewano mkubwa, lakini wakati wa mapumziko niliwaambia wachezaji wangu watulie na wacheze kama nilivyoowaagiza" alisema Engels. 
"Tanzania wanapaswa kuitunza hii timu kwa sababu ina wachezaji wengi chipukizi wenye vipaji vya hali ya juu, ni bahati mbaya tu tumewafunga kwenye penalti. 
Naye beki Erasto Nyoni alisema wamepokea kwa masikitiko matokeo hayo lakini akihidi kuisaidia timu hiyo kwenye michezo mingine. 
"Tunatakiwa kujipanga upya kwa ajili ya mechi za kusaka kufuzu kwa Kombe la Dunia, lazima tukubali matokeo," alisema Nyoni. 
Naye nahodha msaidizi wa Stars, Aggrey Morris alisema hawana kingine zaidi ya kujiuliza wapi walipokosea ili kurekebisha makosa hayo.
Watanzania wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walioneshwa kufurahhishwa na kiwango cha Stars na kusema hata kama wameondolewa, walicheza kwa kujituma.
Anuary Aziz , ambaye anafanya kazi Maputo alisema hajawahi kuona Watanzania wanaoishi nchini hapa wakijitokeza hivyo kushangilia timu  yao na kuongeza kuwa walishapata taarifa kuwa Taifa Stars imeboreshwa.
“Kwa kweli timu imebadilika na kocha huyu asisumbuliwe aachwe afanye kazi yake tumeshindwa lakini vijana wamecheza hadi dakika ya mwisho kwa kweli tumefurahi na tumeshangilia sana. 
“Tanzania tutafika mbali sana tuwe na subira tu kwani wachezaji wetu wanatupa matumaini sana…mchezo huu ulikuwa wa kwetu lakini tumeshindwa kwa penalti tumekubali matokeo na tunajua tutafika mbali,” alisema Mohamed Ali ambaye ni Mtanzania mwingine anayeishi Maputo. 
Stars inategemewa kuwasili Jumanne usiku ikitokea Maputo kupitia Nairobi.

Comments