TBL YAIFAGILIA TAIFA STARS


WADHAMINI wakuu wa timu ya soka ya Tanzania, Kili Taifa Stars, kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager, inaamini timu hiyo chini ya Kocha Kim Poulsen, itafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Hayo yamedokezwa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe (pichani), wakati nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja akimtambulisha rasmi kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo katika chakula cha mchana.
Kavishe alisema, kwa mujibu wa maelezo yaliyomfikia, wachezaji wa Stars walicheza kwa juhudi kubwa katika mechi ya Jumapili iliyopita dhidi ya Ivory Coast, mjini Abidjan, licha ya kufunbgwa mabao 2-0.
 “Nimeelezwa kuwa mlicheza vizuri kwa kujituma na tulikosa nafasi nyingi za kufunga magoli,” alisema Kavishe huku akishangiliwa na wachezaji.
 Alisema kampuni yake inaamini huu ni mwanzo tu na timu ina nafasi ya kupata matokeo mazuri zaidi katika mechi zijazo hasa ya Jumapili dhidi ya Gambia katika vita ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.
 “Lazima tuwafanye watanzania wajione kama sehemu ya timu ya taifa ili watushangilie wakati tunacheza ili ifike wakati walie na sisi tunapolia na wacheke na sisi tunapocheka,” alisema
Aliwaasa wachezaji kuwa karibu na wananchi ili waweze kujisikia kama sehemu yao kwani
watanzania wana matumainai makubwa na timu yao, hivyo ni jukumu la wao wachezaji kuendelea kuwapa matumaini kwa kujituma uwanjani.

Kavishe alisema amefurahishwa na jinsi kocha wa sasa ameweka nidhamu katika timu ya taifa kwani ni jambo muhimu kwa mchezaji wowote. 
Naye kocha wa Timu ya Taifa Kim Poulsen aliishukuru Kampuni ya Bia Tanzania kwa udhamini wake mnono kupitia kinywaji chake cha Kilimanajro Premium Lager na kuongeza uwa timu haiwezi kuwa imara bila udhamini wa uhakika. 
“Kwa sasa tunaweza kufanya mipango ya muda mrefu bila wasiwasi wowote kwa sababu udhamini ni wa uhakika,” alisema. 
Poulsen alisema amefurahishwa sana na udhamini wa Timu ya Taifa na kwamba viwango vya wachezaji vinazidi kuimarika siku hadi siku. 
Mpaka sasa Timu ya Taifa imecheza mechi mbili tangu itangazwe rasmi ya kwanza ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Malawi ambapo timu zote mbili zilitoka sare ya bila kufungana na mechi ya pili ilikuwa dhidi ya Ivory Coast ambayo ilikuwa mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia ambapo Stars ilifungwa 2-0.
Jumapili hii Stars inatarajiwa kucheza na Gambia katika mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia.