WAKATI kikosi cha mabingwa
watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba kikitarajiwa kuondoka jijini
kesho kwenda mkoani Mwanza, uongozi umewapa mapumziko mafupi nyota wake
waandaamizi wanaokipiga katika timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Nyota hao ni pamoja na
Nahodha Juma Kaseja, Haruna Moshi ‘Boban’, Mwinyi Kazimoto na Amir Maftah ambao
walirejea nchini juzi kutoka Msumbuji walipokwenda kucheza na wenyeji wao
‘Mambaz’ katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON)
zitakazopigwa mwakani nchini Afrika Kusini, ambapo ilitolewa kwa mikwaju ya
penalty.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel
Kamwaga alisema jana kwamba wameawapa mapumziko nyota hao ili kujiweka sawa
kwani wamekuwa wakitumika kwa muda mrefu.
Alisema kutokana na mapumziko
hayo, kwenda kwao itategemea na utashi wao wenyewe na kwamba hata mechi za
kanda ya ziwa hawatashiriki kuzicheza.
“Ni kwamba tumeamua kuwapa
mapumziko nyota hawa lakini kama watapenda kwenda Mwanza wataamua wenyewe
lakini huko hawataweza kucheza ile michezo ya kirafiki zaidi ya kushiriki
katika hafla za kutembeza kombe,”alisema.
Simba ambayo inakwenda huko
kwa lengo la kupeleka ubingwa kwa mashabiki wa kanda ya Ziwa jumamosi itacheza
na mabingwa wa ligi kuu soka nchini Uganda, Express jumapili katika uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga, huku Jumamosi itakipiga na Toto African katika
uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kikosi cha Simba kinaendelea
na mazoezi kwenye uwanja wa TCC Chang’ombe chini ambapo mazoezi hayo
yanahusisha wachezaji wa kikosi cha kwanza na wale wa timu ya Vijana.
Comments
Post a Comment