RAIS JAKAYA KIKWETE AIPONGEZA TAIFA STARS


MKuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Saidq akikabidhi bendera

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza wachezaji wa timu ya soka ya Tanzania,
Kili Taifa Stars kuimarika kimchezo hadi kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia
katika mechi ya Jumapili iliyopita kwenye kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Dunia
za mwaka 2014.
Pongezi hizo zilifikishwa kwa wachezaji wa timu hiyo leo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadiq wakati wa hafla ya kuiaga kwenye hoteli ya Tansoma, kabla ya kuondoka
leo kwenda Msumbiji kwa mechi ya kuwania tiketi ya Fainali za Afrika zitakazopigwa mwakani
nchini Afrika Kusini.
Akimnukuu Rais Kikwete, Sadiq alisema, ushindi huo wa Jumapili, umeleta heshima
na kuonesha kuwa wanaweza kama watadhamiria, hivyo waongeze juhudi katika kupigania mafanikio ya timu hiyo katika michuano ya kimataifa.
Stars iliyoagwa jana, inaondoka leo asubuhi kwenda Msumbiji kwa mechi ya
Marudiano itakayochezwa kwesho kwenye Uwanja wa Taifa uliopo katika eneo la Zampeto, nje kidogo ya Jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za huko.
Alisema,ushindi huo umekuwa faraja kwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini
ambao hujitokeza uwanjani kuishangilia na kuwasihi waendelee kutimiza wajibu
wao kwa  timu hiyo iliyo chini ya Kocha Kim Poulsen.
Amewataka wachezaji hao kuzingatia mafunzo ya makocha wao na kuongeza ya kwao huku wakidumisha nidhamu ya ndani na nje ya uwanja ili kupata ushindi katika michezo mbalimbali.
“Nina uhakika mmeandaliwa vizuri, tena kwa kiwango kinachostahili, hivyo ari mliyoonyesha kipindi hiki, iendelee, isionekane kama mmebahatisha…si kwa
Msumbiji tu, bali kwa timu yoyote mtakayokutana nayo,”alisema.
Awali, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodger Tenga aliwasihi nyota hao kuiwakilisha vema Tanzania katika mechi hiyo, wakijituma  wakizingatia mafunzo
na maelekezo ya makocha wao kupata ushindi kwani watanzania wanawategemea.
“Mnakwenda kwenye mechi muhimu sana, tuna imani mtafanya vema kulingana na kiwango kizuri mlichionyesha Jumapili mlipocheza na Gambia, hivyo nina uhakika mtarejea na ushindi na niwatakieni kila la heri,”alisema Tenga.
Naye Poulsen alisema, amekiandaa vema kikosi chake, akinimini watayatumia vema mafunzo aliyowapa kushinda mechi hiyo ambayo anaamini itakuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa.
Alisema, kwa kipindi alichokaa na wachezaji, anafurahi kuona viwango vyao, vimekuwa vikiimarika kila siku, ingawa kuna baadhi ya idara na hasa safu ya  ushambuliaji, imekuwa na udhaifu ambayo inahitaji kazi ya ziada.
“Tunakwenda na akili za kushinda ili kupata mafanikio mazuri huko tuendapo katika mchakato huu wa kusaka tiketi, hivyo ninamatumaini wachezaji watatumia vema mafunzoi yangu na kushinda mchezo huo,”alisema Kim.
Aidha, msafara wa timu hiyo utakaohusisha wachezaji 20 utaondoka bila ya nyota wake watatu ambao ni majeruhi, akiwemo  kipa Mwadini Ali na mabeki Nassoro Masoud Cholo na Waziri Salum.
Kama  Stars itaing’oa Msumbiji, katika raundi ya mwisho itapangiwa moja kati ya timu 16 zilizocheza Fainali za AFCON zilizopita nchini Gabon na Equatorial Guinea ambako Zambia walitwaa ubingwa kwa kuwafunga Ivory Coast.
Katika mechi yao ya kwanza iliyopigwa Februari 29, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, hivyo Stars itapaswa kupata ushindi katika mechi ya kesho kama inataka kusonga mbele.

Comments