MWENYE PINGAMIZI FEKI KUKIONA YANGA SC


KAMATI ya uchaguzi ya klabu ya Yanga imetangaza rasmi majina ya wagombea katika uchaguzi mdogo wa Julai 15, huku ikionya atakayewasilisha pingamizi feki dhidi ya mgombea, atafungiwa na kulimwa faini.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati hiyo, Francis Kaswahili, mwanachama atakayewasilisha pingamizi bila vielelezo, atafungiwa na soka kwa miaka miwili na faini sh 500,000.
Kaswahili alisema, wameamua kuweka tahadhari hiyo kutokana na kasumba iliyojengeka kwa baadhi ya wanachama kufanya hivyo kwa chuki zao binafsi.
Alisema, wakati mwanachama wa aina hiyo akifanya
mzawa kwa kuleta tuhuma zisizo na ushahidi, bado
kamati hupoteza muda wake kuzishughulikia.
Alisema, ingawa hiyo ni sehemu ya kazi yao, lakini ni wajibu
wa mwanachama kuwasilisha pingamizi akijiridhisha kuwa,
ana vielelezo vya kutosha dhidi ya madai yake.
“Hatukatai, mwanachama ana haki ya kumwekea pingamizi mgombea yoyote, lakini pingamizi liwe limejitosheleza kwa maana ya ushahidi wa vielelezo,” alisema Kaswahili na kuongeza:
“Tunatoa tahadhari kwa wanachama mwenye nia ya kuwasilisha pingamizi, afanye hivyo kwa vielelezi, si kwa
chuki binafsi na fitna tu dhidi mgombea, atakayebainika ataadhibiwa,” alisema.
Kuhusu upitiaji wa fomu za wagombea, Kaswahili alisema
limekamilika na keshokutwa watabandika ubaoni majina
ya waliopitishwa kutoa nafasi kwa wenye mapingamizi.
Alisema, mgombea Abdallah Sharia wa Zanzibar, amepewa muda wa kuwasilisha vyeti huku Mohammed Mbaraka akishindwa kuwasilisha cheti cha kidato cha nne.
Alisema kwa nafasi ya Mwenyekiti inayowaniwa na wagombea wanne, wamepita wote ambao ni Yusuf Manji, John Jambele, Edgar Chibura na Sarah Ramadhan.
Waliopita nafasi ya makamu, ni Ayoub Nyenzi, Clement Sanga, Yono Kevela na Ally Mayai Tembele, nyota wa zamani wa Yanga na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
Wajumbe waliopita ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Kampira, Mohamed Mbaraka ‘Binkleb’, Ramadhan Said,
Edgar Fongo, Ahmed Gao na Beda Tindwa, Jumanne.
Wengine ni Mwamenywa, George Manyama, Gadeuncius Ishengoma, Aron Nyanda, Omary Ndula na Shaban Katwila.
Wamo pia Justine Baruti, Jamal Kisongo, Peter Haule,  na Stanley Kevela ‘Yono’ ambaye pia anagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Kaswahili alisema milango ya kuwasilisha pingamizi dhidi
ya wagombea, itafunguliwa kuanzia Juni 14-18, baada ya
hapo kamati yao na ile ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF),  zitapitia.
Uchaguzi unafanyika kuziba nafasi ya Mwenyekiti, Makamu
na nne za ujumbe wa Kamati ya Utendaji baada ya wahusika kujiuzulu na kufariki dunia.
Wakati Mwenyekiti Lloyd Nchunga, Makamu Devis Mosha na wajumbe watatu wakijiuzulu kwa nyakati na sababu tofauti,  mjumbe Thenest Rutashoborwa alifariki dunia hivi karibuni.
Nchunga na wajumbe watatu, walijiuzulu mwezi uliopita kutokana na presha ya wazee chini ya Ibrahim Akilimali
na Bakili Makele kwa upande wa vijana.