KONGAMANO LA MICHEZO KUFANYIKA LEO HOTELI YA BLUE PEAL


WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, leo itaendesha kongamano kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau wa michezo kujadili maendeleo ya michezo. 
Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo, alisema kongamano hilo la siku mbili litafanyika katika Hotel ya Blue Pearl iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam kwa kujumuisha wadau wa michezo. 
Thadeo alisema viongozi wa vyama vya michezo, taasisi za serikali na viongozi wa michezo wa mikoa watapata furasa ya kutoa maoni yao katika kongamano hilo na kisha maoni yatakayotolewa yataingizwa katika sera ya michezo. 
Alisema wizara yake inataka kuona michezo ikiwa na maendeleo na kuhamasisha watu kutumia michezo kwa ajili ya kudumisha amani, kuzuia maambukizi ya magonjwa na pia kwa ajili ya kuimarisha afya zao. 
Alisema kongamano hilo pia litasaidia kutoa elimu ya kujulisha wadau jinsi ya kuelimisha umuhimu wa michezo kwa ajili ya watato kwa ajili ya kuinua vipaji vyao. 
Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, British Council na shirika la Right to Play