KITENDAWILI CHA YONDANI CHAHITAJI UMAKINI MKUBWA


Na Dina Ismail
 GUMZO kubwa kwenye vyombo vya habari takriban kwa wiki nzima iliyopita, ni sakata la beki Kelvin Patrick Yondani wa Simba, kusaini mkataba wa kuichezea Yanga.
Yondani alisaini mkataba huo Yanga Juni 7, akiridhia kukipiga Yanga kwa misimu miwili kwa dau la sh mil. 30.
Baada ya habari hizo kuchapishwa magazetini na picha kumwonesha nyota huyo akisaini,  Simba wakaibuka na kusisitiza, nyota huyo angali wao kwa mujibu kwamba, Yanga imekiuka kanuni za usajili kumsajili mchezaji ambaye bado walikuwa wana mkataba naye huku wakitishia kulifikisha suala hilo Shirikisho la Soka la Kimataifa(FIFA).
Aidha Simba wakaenda mbali wakilitaka  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatilia kwa undani juu ya sakata hilo kubaini mazingira ya nyota huyo kutoka kambini.
Aprili mwaka huu Yondan aliwahi kuhusishwa na mpango wa kujiunga na Yanga, lakini akasema bado alikuwa ni mali ya Simba.
Hata hivyo taarifa za kiuchunguzi na matamshi ya Yondani  mwenyewe ni kwamba aliposaini Yanga alipewa fedha nusu, hivyo ingekuwa rahisi kuwakana.
Kwa kubaini hatari hiyo, Yanga wakafanya jitihada za kummalizia fedha zake na kumpiga picha Yondan akionekana akisani risiti za malipo yake akiwa ana fedha zake mezani, pia kukabidhiwa jezi ya mazoezi, tayari kuanza mazoezi baada ya kuvunjwa kambi ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa Yondan kuonekana akisaini risiti hizo, ilimfanya Mwenyekiti wake, Alhaj ismail Aden Rage, kulaani kitendo hicho, akisema ni cha kihuni kwani hata waliomsainisha, si viongozi wa Yanga.
Rage alimaanisha kuwa mtu aliyehusika kumsajili Yondani, alipata kuwa kiongozi
wa Yanga kabla ya kujiuzulu, hivyo sheria na kanuni za soka hazimpi uhalali mtu wa aina hiyo.
Rage anaongeza kuwa mkataba wa Yondani kwa Yanga ni batili, kwani awali ulionyesha amezaliwa mwaka 1994, hivyo ana umri wa miaka 17; kwa sheria za kazi, umri huo haruhusiwi kusaini mkataba.
Hata hivyo, Yanga waliifanyia kazi dosari hiyo kwa kubadili, wakiandika kuwa amezaliwa mwaka 1984.
Rage anasema, mkataba wa Yondani ni kiini macho kwani umeficha baadhi ya vipengele, huku pia ikionyesha kuwa atalipwa fedha zake kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza, ni Desemba 30, 2013 na awamu ya pili itakuwa Februari 30, hivyo ni sawa na kusema, atacheza bure Yanga.
Akifafanua zaidi juu ya mchezaji huyo aliyezaliwa Oktoba 9, 1984, Rage anasema, mkataba wake awali ulikuwa ufikie ukomo Mei 30, 2012, lakini Desemba 23, 2011, waliurefusha kwa miaka miwili zaidi, hivyo kucheza Simba hadi mwaka 2014.
Kwa mantiki hiyo, mkataba mpya wa Yondani kwa Simba, ulianza kutumika Juni mosi, 2012, lakini usiku wa Juni 7, akasaini kuichezea Yanga.
Simba waliwasilisha malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tayari Rais wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga, ameahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo kujua kama Yondan aliondoka kambi ya Taifa Stars kwa ruksa au alitoroka.
Tenga amewaahidi Simba, ikibainika Yondan alitoroka kambini hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa wahusika wote.
Hata hivyo baada ya Simba kuja mbogo juu ya suala hilo, Yondan mwenyewe alikaririwa kukisisitiza ni mali halali ya Yanga, amesaini mkataba wa miaka miwili kwa kitita cha sh mil 30 na mshahara wa 800,000 kwa mwezi.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na familia yake ambayo pamoja na kukiri ndugu yao huyo kusaini Yanga, imeweka bayana soka ni ajira yake, hivyo hakuna ubaya wa Yondani kuangalia hatma ya mustakabali wake.
Kwa maelezo hayo yaliyotolewa na watu wenye akili timamu kusema kuwa hajasaini Simba, amesaini Yanga ni wazi kuna walakini kwani awali alisema hajasaini Yanga, ameongeza mkataba na klabu yake Simba!
Ikumbukwe, suala la Yondan na Yanga si la jana wala juzi, mchezaji huyo kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kujiunga na
klabu hiyo ya Jangwani.
Hii ilifanya Yondani kutoaminiwa kwa asilimia 100 na Simba kwa madai kuwa alikuwa na mapenzi na Jangwani.
Mashabiki wenyewe wa Simba wamekuwa hawamkubali mchezaji huyo linapokuja suala la Yanga- kama ilivyokuwa kwa kiungo na Nahodha wao wa zamani, Henry Joseph Shindika, ambaye kwa sasa anacheza nchini Norway.
Lakini, Yondan alifanya mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kuhamia huko, tangu mwaka 2008 enzi hizo klabu hiyo ikiwa chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic, ingawa hawakufanikiwa.
Yanga wamekuwa wakirudi tena na tena kwa Yondan bila mafanikio, na kwa sababu hiyo, hili si suala la kushtukiza na iko siku  beki huyo atacheza Yanga hata kama
si msimu ujao.
Lakini, hata kama Yondan ana mapenzi na Yanga, akibainika kusaini Yanga wakati bado ana makataba na Simba, itamgharimu yeye kwanza na Yanga wenyewe.
Kwa upande mwingine, Yondan anaweza akaamua kwenda Yanga licha ya kuwa na mkataba na Simba kutokana na hukumu ambayo tayari amekwishapewa siku nyingi na mashabiki wa Simba.
Hukumu yenyewe ni kumwona kama si mwenzao, wahenga walisema, lisemwalo lipo, kama halipo, linakuja!
Lakini, yamekwishatokea masuala ya kuumiza kichwa kama hili la Yondani kusaini mara mbili tena wakati huo kukiwa hakuna kanuni madhubuti, lakini yakapatiwa ufumbuzi.
Hapa namaanisha, jambo hili la Yondan linaweza kumalizwa kwani limekuja kipindi ambacho, kanuni za usajili zimekaa vizuri.
Sakata hili ni kama ilivyokuwa kwa Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka Simba kwenda Yanga mwaka 2007.
Wakati huo, Yanga ilipomsajili Chuji, Simba nayo ikasema ni wao kwa mujibu wa mkataba, lakini mwishowe, alicheza Jangwani.
Naye Victor Costa alisaini Yanga akitokea Simba, akavaa jezi kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar, aliporejea Dar es Salaam akaenda kwenye mazoezi ya Simba Kurasini, mwaka 2005.
Amri Saidi alisaini Yanga mwaka 2001, lakini pamoja na kupewa fedha, akabaki Simba.
Ephraim Makoye  alisaini Simba mwaka 2000, lakini akabaki Yanga ingawa baadaye alicheza Simba.
Leo hii, kuna Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, pia Kamati ya Nidhamu ya TFF, kutoka kwao tunatarajia watalipatia ufumbuzi hili la Yondan.
Baada ya hapo, tutakuwa na fursa nzuri ya kufungua mjadala mpya.
Hata hivyo, jambo hili la Yondani, ni kitendawili kigumu kinachohitaji umakini kukitegua. Ngoja tusubiri kuona.
 Maoni:dinazubeiry@gmail.com, 0788-344 566 au tembelea http//:mamapipiro.blogspot.com