KAMATI YA UCHAGUZI YANGA 'YAFUNGUKA'


WAKATI kamati ya uchaguzi ya Yanga ikitupilia mbali pingamizi la mwanachama Abeid Falcon, kamati hiyo kesho inatarajiwa kusikiliza pingamizi walizowekewa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Julai 15. 
 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji John Mkwakwa (pichani) amesema wametupilia mbali pingamizi la Falcon kutokana na kutokuwa na mashiko yoyote. 
Alisema kamati yake inashangazwa na Falcon kupinga katiba ya klabu hiyo ambayo aliwahi kugombea uenyekiti mwaka 2010 akitumia katiba ya mwaka huo ambayo iliwasilishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Juni 17, 2010 na kusajiliwa kwa msajili wa vyma vya michezo. 
Aliongeza kuwa kamati yao inaendelea na mchakato wa uchaguzi ambapo leo itasikiliza pingamizi walilowekewa wagombea Yusuf Manji (mwenyekiti), Stanley Yono Kevela, Ali Mayay na Clement Sanga wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti. 
Mkwawa alisema baada ya zoezi hilo wanatarajiwa kuwafanyia usaili wagombea Juni 22 na 23, hivyo amewaomba wanachama kufuata taratibu zilizowekwa katika mchakato huo. 
“Tufanya kazi kwa miongozo iliyowekwa na si kwa shinikizo la mtu au kikundi cha watu, hivyo tunawaomba wanachama na kufuata taratibu hizo,”alisema Jaji Mkwawa.