JERRY TEGETE AIZODOA SIMBA SC


KLABU ya soka ya Yanga imewapiga tena bao la kisigino mahasimu wao wa jadi nchini Simba baada ya  kumuongezea mkataba wa miaka miwili nyota wake  Jerryson Tegete.
 Wakati ligi kuu soka Tanzania Bara ikielekea ukiongoni, Simba ambao ni mabingwa wa ligi hiyo walianza mpango wa kutaka kumsajili mchezaji huyo baada ya kuwepo taarifa kutoka Yanga kwamba haina mpango naye tena.
 Hata hivyo, baada ya tetesi za Simba kumuwania Tegete kuzagaa mtaani ndipo Yanga iliporudi nyuma na kuamua kumfunga mchezaji huyo ambaye mkataba wake ulikuwa unalizika mwezi huu hadi mwaka 2014.
 Mmoja ya wadau wa Yanga wanaohusika na usajili wa wachezaji katika klabu ya Yanga alisema jana kwamba wameamua kumbakiza kundini Tegete kutokana na umuhimu alionao katika kikosi hicho.
 “Napenda niwatoe shaka wanayanga kwamba kwa Tegete ataendelea kuvaa uzi wa njano na kijani kwa miaka miwili…wale walikuwa wakimuwania nawapa pole kwani ameshamwaga wino jangwani,”alisema.
 Tegete ambaye  msimu uliopita hakuweza kung’ara  alitua Yanga mwaka 2008, akitokea sekondari ya Makongo, ambapo kutokana na umahiri alionao kwa nyakati tofauti alipata kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
 Yanga ambayo kwa sasa imeingia vita na Simba baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili nyota wake Kelvin Yondan ‘Vidic’, pia imeshamsajili kipa wa Simba  Ally Mustafa  ‘Barthez’ ikionekana kama kulipa kisasi baada ya Simba kumsajili  Kiggi Makassy.