HATIMAYE filamu ya ujio wa
aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Mbrazil Marcio Maximo kujiunga
na klabu ya Yanga imefikia tamati jana baada ya uongozi kutarajia kumtangaza
kocha mpya wiki ijayo.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga Mwesiga Selestine alisema kocha huyo atatoka
katika nchi zilizopo Amerika Kusini au Ulaya.
Alisema uongozi ulipitia
maombi ya makocha 25 waliotuma wasifu zao kwa ajili ya kutaka kibarua katika
klabu hiyo ambapo wamewachuja na kubaki watano.
Akizungumzia suala la Maximo,
Katibu huyo alisema wameamua kuachana naye kwa vile bado ana mkataba na klabu
yake ya Democrata FC ya Rio de Janeiro,Brazil huku pia akipata ofa za
kufundisha timu mbalimbali za Taifa ikiwemo timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’.
“Kwa sababu hizo isingekuwa
rahisi kumchukua Maximo kufundisha Yanga, kwa mantiki hiyo tumeshafanyia mchujo
maombi na kubaki makocha watano ambapo mmojawapo ndiye atakayekuja kuinoa
Yanga,”alisema.
Hivi karibuni Yanga
ilitangaza ujio wa Maximo nchini kwa ajili ya kurithi mikoba ya Mserbia
Kostadin Papic ‘Clinton’ ambaye alitupiwa virago miezi michache kabla ya
kumaliza mkataba wake kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo.
Hata hivyo kadiri siku
zilivyokuwa zikisonga mbele ujio wa Maximo
ulibaki kuwa ‘kiza kinene’ huku uongozi ukishindwa tena kuweka wazi
kilichosababisha kocha huyo ashindwe kutua nchini kama walivyotangaza awali.
Katika hatua nyingine,kikosi
cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Kaunda chini ya kocha
msaidizi Fred Felix Minziro, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya kagame
inatotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14.