FM ACADEMIA NA USIKU WA WINDHOEK IJUMAA, ARCADE


BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, wanatarajia kufanya vitu adimu kwenye shoo iliyopewa jina la ‘Usiku wa Windhoek na Ngwasuma’, itakayofanyika Ijumaa ya Juni 22, katika Ukumbi wa Arcade, Mikocheni,  jijini Dar es Salaam.
Katika shoo hiyo, watu mia wa kwanza watapata bia moja bure, huku burudani za nyimbo za wakali wa Ngwasuma zikitarajiwa kuwa za aina yake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Kelvin Mkinga, alisema kwamba mashabiki watapata burudani kali kutoka kwao, hivyo ni wakati waop kuingia kwa wingi kujipatia shoo za aina yake.
Alisema FM Academia ni bendi imara zenye mashabiki lukuki, hivyo wanaamini watafurahia burudani zao, walizozipa jina la ‘Usiku wa Windhoek’.
“Mashabiki wetu waje kwa wingi katika shoo yetu ili wapate burudani kamili, kutoka kwa nyimbo zetu mpya na zile za zamani ambazo zipo kwenye kiwango cha juu.
“Naamini mambo yatakuwa mazuri, ukizingatia kwamba wanamuziki wetu wamejipanga imara kuwapatia vitu vya hali ya juu, ili kuiweka juu bendi zaidi bendi yetu,” alisema.
FM Academia inaongozwa na Rais wa Vijana, Nyosh Al Sadaat, akishirikiana na wakali mbalimbali wanaofanya makubwa katika bendi hiyo ambayo pia inajulikana kwa jina la Wazee wa Pamba.