ETHIOPIA YATUA TAYARI KUIKABILI TWIGA STARS J'MOSI


Msafara wa watu 25 wa timu ya Taifa ya wanawake ya Ethiopia umewasili leo (Juni 14 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwa ajili ya mechi dhidi ya Twiga Stars.
 
Mechi hiyo ya marudiano kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea itachezwa Jumamosi (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
 
Mshindi baada ya matokeo ya mechi ya awali ambapo Twiga Stars ilifungwa mabao 2-1 na mechi ya Jumamosi atafuzu kwa fainali hizo za Equatorial Guinea.  Nchi ambazo tayari zimefuzu kwa fainali hizo ni wenyeji Equatorial Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
 
DRC ilikuwa icheze raundi ya pili na Equatorial Guinea, lakini baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuipa uenyeji Equatorial Guinea, DRC nayo imefuzu moja kwa moja kucheza hatua hiyo ya fainali.
 
Makocha wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa na mwenzake wa Ethiopia, kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF kuelezea jinsi timu zao zilivyojiandaa kwa mechi hiyo.
 
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A na sh. 5,000 kwa VIP B na C. Sehemu nyingine zilizobaki kiingilio ni sh. 2,000 na tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi kuanzia saa 3 asubuhi.