KAMATI ya utendaji ya klabu
ya Yanga inatarajiwa kukutana kesho kwa ajili ya kujadili ripoti ya kamati ya
ufundi ya timu hiyo, imefahamika.
Mwenyekiti wa Yanga Lloyd
Nchunga ameiambia mamapipiro blog kwamba kwamba kamati ya mashindano chini ya mwenyekiti wake
Mohammed Bhinda inatarajiwa kukutana jioni ya leo kwa ajili ya kuandaa ripoti hiyo.
Alisema kuwa mara baada ya kupitia na kuijadili ripoti hiyo
ndipo hatua nyingine zitafuata kabla ya kuziwasilisha rasmi kwa wanachama wa
klabu hiyo.
Nchunga na kamati nzima ya
utendaji ya Yanga ilijikuta katika wakati mgumu hivi karibuni baada ya timu
hiyo kuonyesha mwenendo mbaya wa ligi hiyo na hatimaye kupoteza ubingwa wake
iliyokuwa ikiushikilia.
Yanga ambayo ilimaliza ligi
hiyo ikiambulia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49 juzi ilimaliza ligi hiyo kwa
kupokea kipigo cha mabao 5-0 toka kwa mahasimu wao wa jadi Simba ambao walitwaa
ubingwa.
Kufanya vibaya kwa Yanga
katika ligi kuu kulipelekea baadhi ya wanachama kuutaka uonmgozi ujiuzulu,ambapo
Nchunga aliwataka wanachama kusubiri ligi imalizike kwanza na uongozi ufanye
tathmini ndipo wachukue hatua zinazostahili.
Aidha, katika sekeseke hilo wajumbe wawili wa
kamati ya utendaji Sarah Ramadhan na Seif Ahmed walitangaza kuachia ngazi, pia
mjumbe wa kamati ya usajili na mashindano ya klabu hiyo Abdallah Binkleb naye
kujiengua.
Kama hiyo haitoshi, Baraza la
wazee wa klabu hiyo lilitangaza kuichukua timu wiki moja kabla ya kumalizika
kwa ligi kwa madai kuwa walikubaliana na Nchunga, lakini baadaye mwenyekiti
huyo alikana suala hilo
na kusema kuwa hawezi kukabidhi timu kwa watu asiokuwa na uhakika nao.
Kauli hiyo ya Nchunga
iliwachukiza wazee hao ambao waliamua kumvulia kofia Nchunga huku wakidai
kusikitishwa na kauli za fedheha ambazo zilikuwa zikitolewa na Nchunga dhidi yao .
Comments
Post a Comment