Kwa mujibu wa blogu ya Bongo Starz:
MVUA inanyesha,
lakini mamia ya watu wamejazana mchana huu nje ya nyumba aliyokuwa anaishi
marehemu Steven Charles Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia
leo.
Nyumba hiyo ipo eneo
la Sinza, mkabala kabisa na hoteli maarufu ya Vatican. Pande zote mbili za
barabara inayotokea Sinza Kijiweni kuelekea Tandale Uzuri watu
wamejazana.
Misururu ya watu
imeanzia kwenye hoteli ya Deluxe, Sinza na wengine ambao wameamua kujiweka
kwenye baa zilizo jirani na eneo hilo ili mradi washiriki kwa namna
yoyote.
Nyumba zilizo jirani
na nyumba aliyokuwa akiishi The Great Kanumba watu wamepanda juu ya kuta
kuchungulia ndani ya nyumba ya staa huyo, nini kinaendelea.
Yote haya yanaashiria
ni kiasi gani Steven Kanumba alikuwa kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini.
Kipenzi cha Watanzania.
Vilio, manung’uniko,
sura za majonzi na simanzi, vyote vimetawala eneo la tukio. Hakika ni majonzi
makubwa- na hata baadhi ya wanaume wanashindwa kujizuia. Wanalia. “Kanumba,
Kanumba, why Lulu?” alisikika dada mmoja akisema huku analia, karibu kabisa na
geti la nyumba aliyokuwa akiishi marehemu.
Ndani ya nyumba hiyo,
watu hawaingii tena. Kumejaa. Getini kuna ulinzi mkali na idadi ya watu
waliojazana getini ni sawa ile misururu ya kuingia kwenye mechi kubwa Uwanja wa
Taifa.
Maoni ya watu ni
kwamba, eneo ambalo watu wamekusanyika kwa sasa ili kuomboleza msiba huo
halitoshi na wanapendekeza msiba huo upewe hadhi ya kitaifa kwa kupelekwa kwenye
maeneo ya wazi.
KIFO
CHAKE:
![]() |
| Kanumba |
Kanumba alifariki
dunia ghafla usiku wa kuamkia leo na chanzo cha kifo chake inaelezwa ni
kugombana na mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Lulu.
“Alikuwa anagombana
na Lulu. Lulu akamsukuma Kanumba, akaangukia kichwa, ndio akafa, ilikuwa saa
tisa usiku,” kilisema chanzo.
Habari zaidi
zinasema, wivu ndio chanzo cha ugomvi wao.
Inaelezwa Lulu
alikuwa anazungumza na simu na Kanumba akataka kujua anaongea na
nani.
Lulu hakutaka kumpa
simu Kanumba na ndipo wakaanza kuvutana na mwenzake akadondoka
chini.
Inaelezwa alidondokea kisogo katika
eneo gumu na ndipo hali ikawa mbaya kabla ya kifo chake.
MWILI WA
KANUMBA:
![]() |
| Waombolezaji |
Kwa sasa mwili wa mwigizaji huyo wa picha la Big Daddy upo katika vyumba vya kuhifadhia maiti, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mwili huo
ulichukuliwa mara tu baada ya tukio lililosababisha kifo
chake.
Kanumba ambaye filamu
yake ya mwisho kuingia sokoni ni Tambua Haki, inayoendelea kuuzwa hivi sasa,
imeelezwa kwamba Lulu ndio chanzo cha kifo chake.
Ndugu wa Kanumba ambaye alikuwa akiishi naye
Sinza, jijini Dar es Salaam na wakati mauti yanamkuta- na aliyekuwapo nyumbani
amethibitisha hayo alipohojiwa na waandishi wa
habari.
Ndugu huyo
amekaririwa akisema Lulu ambaye jina lake halisi ni Elizabeth Michael, alikuja
nyumbani kwa Kanumba na kumkuta yeye (ndugu) amekaa na marehemu
usiku.
Ndugu huyo anasema aliwaachia faragha
wawili hao wazungumze, lakini baada ya muda akasikia malumbano na yalipozidi
wakahamia chumbani, ambako waliendelea kugombana.
Anasema baada ya
muda, Lulu alitoka chumbani akipiga kelele huku akimuita yeye
(ndugu).
Anasema alipotokea,
Lulu akasema Kanumba ameanguka chumbani na povu linamtoka
mdomoni.
Ndugu huyo anasema alipokwenda
chumbani, kweli alikuta hali hiyo, akaenda kumuita
daktari.
Anasema aliporejea na daktari, katika
hali ya kushangaza, akakuta Lulu amekwishatoweka, ndipo wakachukua mwili wa
marehemu na kuupeleka Muhimbili.
LULU YUKO WAPI?
| Kimwana Lulu |
Tayari Lulu amekwishakamatwa na Polisi na amehifadhiwa Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam.
Chanzo cha habari
kinasema Lulu amechanganyikiwa na tangu ahakikishiwe kwamba Kanumba amefariki
dunia, hajitambui.
Bado ni kizungumkuti
juu ya hatima ya Lulu na kifo cha Kanumba na ni taarifa ya Polisi pekee
itakayoondoa utata kuhusu tukio zima hilo.
Ingawa siri ya
mapenzi yao inafichuka baada ya kifo cha mwenzake, lakini Lulu katika mahojiano
mbalimbali ambayo amekuwa akifanyiwa amekuwa akikakana kuwepo uhusiano wa aina
yoyote kati yake na marehemu Steve.
MSIBA,
MAZISHI:
![]() |
| Ndani kwa Kanumba |
Bado pamoja na mvua
kunyesha, eneo dogo, lakini bado watu wanakusanyika Sinza.
Ndani ya nyumba
waliobahatika kuingia kwa wingi ni wasanii mastaa haswa, na watu wa karibu,
lakini wengine wamekwama nje.
Kulingana na umaarufu
wa Kanumba katika jamii, familia ya marehemu italazimika kushirikiana na
serikali kupitia vitengo husika kama BASATA katika kuratibu mazishi ya nyota
huyo aliyekuwa na kipaji kikubwa cha uigizaji.
Ni moja kati ya mawili, Kanumba
atasafirishwa Shinyanga au atazikwa hapa hapa Dar es Salaam. bongostaz
inaendelea kufuatilia kwa karibu na itaendelea kukupasha kila kitakachojiri.




