SERIKALI YAIPIGIA DEBE TWIGA STARS


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeipongeza Kampuni ya Heineken Afrika Mashariki kwa kuiteua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotembelewa na Kombe la UEFA, huku ikiiomba kuwekeza kwenye sekta ya michezo hapa nchini hususan, timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Pongezi na maombi hayo yalitolewa juzi usiku na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, katika hafla ya kulishuhudia kombe hilo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es Salaam.
Dk. Mukangara alisema wanatambua uwepo wa Heineken hapa nchini, kwani wanaziona bidhaa zao, hivyo kwa namna moja ama nyingine wanachangia uchumi wa nchi kupitia kodi.
Alisema kwa uamuzi huo wa kulileta kombe hilo maarufu duniani, wameongeza chachu na hamasa ya michezo hapa nchini, lakini litakuwa jambo bora kama watawekeza kwenye michezo hapa nchini na kuisaidia Twiga Stars, hasa ukizingatia inajituma na kuonyesha kiwango bora.
Katika hafla hiyo, ambayo waalikwa walipata nafasi ya kupiga picha na kombe hilo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mathias Chikawe, Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Cheyo, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake, Lina Madina Mhando na wengineo. 

Comments