TWANGA PEPETA NA VALENTINES YAO LEO EQUATOR GRILL


Na Mwandishi Wetu

Bendi ya Twanga Pepeta `Wazee wa Kisigino’ leo usiku itatambulisha vibao vyao vipya wakati watakapotumbuiza kwenye onyesho la Valentine Day katika ukumbi wa Equator Grill, Temeke.

Onyesho hilo limeandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment chini ya udhamini wa Dodoma Wine na Freditto Entertainment.

Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka, alisema jana kuwa watatumia onyesho la leo kutambulisha nyimbo zao mpya ambazo zitakuwepo kwenye albamu mpya.

“Mbali na kutambulisha nyimbo hizo pia tutapiga nyimbo zetu zote za zamani pamoja na zile zilizopo kwenye albamu yetu mpya ya Dunia Daraja,” alisema Asha.

Asha aliwaomba wapenzi wa muziki wajitokeze kwa wingi ili wasikilize tungo zao mpya na rapu mpya.

Naye mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga, amesema ulinzi utaimarishwa kwenye onyesho hilo.

“Tutakuwa na ulinzi mkali utakaongozwa na polisi, maninja na mabounsa,” Kapinga alisema.

Alifafanua kuwa hatua ya kuimarisha ulinzi imetokana na onyesho hilo kwenda sambamba na siku ya wapendanao ambapo, waandaaji wataweka ulinzi ndani na nje kwa usalama zaidi wa mashabiki wa muziki watakaoingia katika onyesho hilo.

Kapinga alisema kutakuwa pia na zawadi mbalimbali itakayotolewa kwa mashabiki wa bendi hiyo inayotamba na staili ya `Kisigino.’

Albamu ya mwisho ya “Dunia Daraja” inayotamba sasa hivi ina nyimbo kali kama Mapenzi Hayana Kiapo, Penzi la Shemeji, Mtoto wa Mwisho, Umenivisha Umasikini, Kauli na Dunia Daraja.

Bendi hiyo inaundwa na wanamuziki machachari kama akina Dogo Rama, Msafiri Diouf, Amigolas, Haji, Vena, Saleh Kupaza, Luiza Mbutu, Khadiji Mnoga na Janet Isinika na Muumin Mwinjuma katika safu ya uimbaji.

Katika safu ya upigaji vyombo wapo

Jojo Jumanne, Thabiti Abdul, Miraji Shakashia, Gody Kanuti, Kado, Victor Mkambi, James Kibosho, MCD na wengineo

Katika upande wa unenguaji wapo

Super K, Saidi, Mandela, Abdilayi Zingu, Asha Sharapova, Lilian Enternet, Maria Soloma, Vicky na Regina.

Kwa upande wake Dogo Rama amesema wamejiandaa vya kutosha kuwapa burudani wapenzi wao burudani ya kiwango cha juu.

Comments