BANGO LA BURE TOKA TFF HAKUNA KULIPISHWA

MANYONI FC YASHUKA DARAJA

Timu ya Manyoni FC ya Singida imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ichezwe juzi (Februari 12 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya FDL timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.
Si Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Tabora, Alfred Sitta wala Kamishna wa mechi hiyo Charles Komba waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya Manyoni FC kushindwa kufika kituoni.

Manyoni FC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao ilikuwa Kundi C pamoja na timu za 94 KJ ya Dar es Salaam, AFC ya Arusha, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.

LIGI KUU YA VODACOM

Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 18 kesho (Februari 15 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazochezwa viwanja vya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha, Azam Chamazi jijini Dar es Salaam, Mkwakwani jijini Tanga na Kaitaba mjini Bukoba.

Mwamuzi Israel Mujuni atazichezesha JKT Oljoro na Ruvu Shooting jijini Arusha, Azam na Villa Squad zitachezeshwa na Judith Gamba jijini Dar es Salaam, Oden Mbaga ndiye atapuliza filimbi kwenye mechi ya Coastal Union na JKT Ruvu jijini Tanga. Mjini Bukoba kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Moro United.

Mechi nyingine ya raundi ya 18 itachezwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Toto Africans itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Timu nane zinaingia viwanjani kesho (Februari 15 mwaka huu) kusaka pointi tatu katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo sasa iko katika mzunguko wa pili hatua ya makundi.

Kundi B ni kati ya Majimaji na Small Kids zitakazooneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati Mbeya City itaumana na Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za Kundi C zitakuwa kati ya Polisi Morogoro na Polisi Tabora kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku 94 KJ ikiwa mwenyeji wa AFC katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi ya Kundi A kati ya Mgambo Shooting na Polisi Dar es Salaam jijini Tanga. Februari 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo kutakuwa na mechi kati ya Transit Camp na Morani ya mkoani Manyara.
Mechi nyingine ya Kundi B itapigwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) ikizikutanisha timu za Tanzania Prisons na JKT Mlale kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Boniface WamburaOfisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)




Comments