SIMULIZI YA MAMAPIPIRO HII HAPA !






MWEZI MMOJA



MIEZI MIWILI



MIEZI MITATU



MIEZI MINNE



MIEZI MITANO


LEO NI SIKU YA KUZALIWA KWA MTOTO WANGU WA TATU PRINCE AKBAR, PAMOJA NA KUSHEREHEKEA HUO ITAKUWA NI VEMA KUKUMBUKA MATATIZO NILIYOKUMBANA NAYO KABLA YA KUJIFUNGUA KWA OPERESHENI JULAI 28 KATIKA HOSPITALI YA TUMAINI, UPANGA JIJINI DAR ES SALAAM.


NATAMANI kukutana ana kwa ana na Waziri Afya na Ustawi wa Jamii Profesa David Mwakyusa na kumwambia kila kinachoendelea kuhusiana na unyanyasaji wanaofanyiwa wakinamama wajawazito ambao wanasubiri kujifungua katika hospitali ya Amana.


Natamka hivyo kwa sababu nitakapopata nafasi hiyo nitamueleza kile nilichokishuhudia kwa macho yangu katika wodi ya wazazi hospitalini hapo wakati nilipokuwa mmoja ya wazazi wanaosubiri huduma hiyo.

Nadhani ningepata nafasi ya kuonana na Prof. Mwakyusa ningemshauri kuwafuta kazi ama kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika wote wa wodi hiyo ikiwemo viongozi wao.

Na hiyo inatokana na kwamba kwa asilimia kubwa watu hao wamekuwa wakichangia kwa namna moja ama nyingine kusababisha vifo vya kinamama au watoto wachanga kutokana na uzembe wao.

Ingawa tumekuwa tukiambiwa kuwepo kwa sababu mbalimbali za kusababisha vifo hivyo lakini sababu hiyo ni mojawapo na iwapo kutafanyika jitihada kubwa nadhani idadi itapingua kwa asilimia 50.

Mimi kama mwandishi wa habari nimekuwa nikisoma habari zilizoandikwa na wanahabari wenzangu kuhusiana na matatizo wanayokumbana nao wakinamama wanaokwenda kujifungua hospitalini hapo ambao wamekuwa wakipatwa na matatizo mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo niliiweka msimamo kichwani kwangu kuwa katika maisha yangu nisingethubutu kwenda kujifungulia hospitalini hapo lakini ahadi zote haziwezi kutimia kwani mwenyezi mungu ndiye mpangaji.

Unajua ilikuwa vipi, siku moja nililala hospitalini hapo baada ya kuhamishwa kutoka katika hospitali moja binafsi baada ya kushindwa kunipatia huduma hiyo kutokana na kuzidiwa uwezo wa kitaalamu.

Nilihamishiwa Amana baada ya kuwekewa chupa mbili za maji ya uchungu huko nilipotoka bila mafanikio hivyo waliona ni busara kupelekwa hospitali ya Wilaya kwa ajili ya huduma za kitaalamu zaidi.


Nakumbuka nilifikishwa pale (Amana) majira ya saa nne kama na nusu usiku, nilipofika kwanza nilivyopokelewa tu niliona kama nimefikishwa mahabusu kwani wauguzi wa zamu hawakuwa na lugha nzuri hata kidogo.

Hali niliyoiona, yaani wagonjwa kulala wawili kitandani, uchafu wa vyoo navyo vilinifanya nikose amani ya kuwepo mahala hapo na kutamani kurudi nyumbani na ndugu zangu lakini ilishindikana kutokana na kuwa tayari nilishakabidhiwa kwa wauguzi.

Pamoja na kauli zisizo za kistaarabu toka kwa wauguzi nilizozipata mimi pamoja na wakinamama wenzangu, pia huduma haikuniridhisha kwani niliishia kupimwa njia tu na kisha kupewa kitanda.

Hali ile ilinifanya nikose hata chembe ya uchungu, nilijisikia ubaridi na nilijihisi kupooza kwa viungo vyote,mapigo ya mtoto tumboni yalipotea, usiku mzima tulikuwa tukizungumza mambo mbalimbali na wenzangu wodini pale.

Nilikuwa nikitamani kukuche ili niondoke kwa njia yoyote ile, lengo ikiwa ni kwenda kuyanusuru maisha yangu na ya kiumbe mtarajiwa kwani kuendelea kulala pale niliona nakikaribisha kifo, tena kifo cha kujitakia.

Huduma waliyokuwa wanakazana kuitoa ni kupima njia, mwanamama akilalamika kitu kuhusiana na tumbo ni kwenda kupima njia, nilishangazwa na hali hiyo na hapo nikapatwa na ujasiri wa kuwa mkaidi ili nione matokeo yake.

Sikuona sababu ya mtu kupimwa njia kila wakati wakati sababu nyingine zilizowapeleka kinamama wodini hapo hazikuhitaji hata kupimwa njia.

Mfano mtu ana ujauzito miezi sita anatokwa mabonge ya damu, ama ana ujauuzito wa miezi nane chupa imepasuka, hata mimi ambaye uchungu ulipoa kabisa ambaye umri wa mamba ulifika zaidi ya wiki 40 nilitakiwa kupima njia pia!

Na kwa kamchezo hako baadhi ya kinamama walijifungua kwenye kitanda cha kupimia badala ya leba, wengine walijifungua chini na wengine vitandani walipolala yote ni sababu ya uzembe wa wauguzi.

Niliwaona wauguzi hao hawafai kabisa ambako nikiwa na baadhi wa wanawake tuliingiwa na hofu kubwa kiasi cha kupanga mikakati ya kutoroka kesho yake kama tusingeruhusiwa.

Kulipokucha alikuja muuguzi mmoja na kutangaza kuwa kila mmoja awe tayari kwa kuonana na daktari, ilipofika zamu yangu niliiingia na daktari alinitaka nipande kitandani kwa ajili ya kupima njia, nilimkatalia na kumwambia haiwezekani kwani uchungu umepoa, pia nilikuwa ninamaumivu makali na michubuko yaliyotokana na kupimwa njia kila mara.


Daktari aliniambia “naona huumwi hiuvyo inabidi urudi nyumbani mpaka pale utakapopatwa na uchungu tena”, nilimkubalia na hapo hapo nikawasiliana na ndugu zangu kuwa wakija mchana tunaondoka pamoja.

Yule daktari alinishangaza sana, mimi pamoja na kutokuwa mjuzi wa masuala ya kitabibu nilimuona daktari yule hafuati miiko ya kazi, kwani aliyoyafanya ni makosa makubwa na hasa ikizingatiwa vyeti vilijieleza wazi na ilitakiwa huduma ya maana si kupima njia.


Nilipotoka mchana ule nilipelekwa moja kwa moja na kupelekwa hospitali binafsi ya Tumaini na nilifanyiwa uchunguzi wa haraka na kubainika kwamba mtoto alikuwa mkubwa hivyo isingewezekana kujifungua kwa njia ya kawaida.


Pia ilibainika kuwa mtoto alishachoka kwani hata kama njia ingefunguka wakati huo asingeweza kujisaidia kutoka na hivyo zilifanyika jitihada za haraka kuokoa maisha yake kwa kumtoa kwa njia ya upasuaji.

Awali ya hapo, daktari huyo bingwa aliyenihudumia alinieleza kuwa mama anapowekewa maji ya uchungu hatakiwi kutolewa chupa zile na hubaki vilevile labda afanyiwe njia nyingine ya kumzalisha.

Namshukuru mwenyezi mungu, baada ya kuzinduka kesho yake nilikabidhiwa mtoto wa kiume ambaye alikuwa na kilo tano na gramu kadhaa.

Baada ya hatua hiyo nilikujabaini kuwa ubishi wakati mwingine unasaidia, pia kujitambua kuwa una hali gani kunaweza kukuepusha na mabalaa ambayo yanaweza kuepukika.


Mathalani ningeendelea kulala Amana nadhani ingekuwa hadithi nyingine, ningepoteza maisha mimi au mtoto ama wote, kifo ambacho kingetokana na uzembe wa wauguzi.


Kwa mchakato huo nimebaini kuwa ni kweli uzembe wa wauguzi ama watoa huduma za afya unachangia vifo vya kinamama wajawazito ama watoto kwani kwa kesi kama yangu ni wazi kuwa kifo kilikuwa kinaninyemelewa ingawa kila siku namtanguliza Mwenyezi Mungu.

Naungana na wanawake wenzangu ama watatanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha, kupata matatizo wao ama watoto wanaozaliwa kutokana na uzembe wa namna hiyo.

Ndiyo maana tangu hapo nilisema lazima nitakapomaliza likizo ya uzazi, nitaandika makala inayoelezea adha wanazokumbana nazo wajawazito wanapokwenda kujifungua katika hospitali hizo.

Napenda kuwathibitishia Watanzania na Waziri Mwakyusa yanayoandikwa na vyombo vya habari kuhusiana na hospitali hiyo yana ukweli mtupu wala hawasingiziwi hivyo Mh.Mwakyusa kazi ya kuondoa uozo huo ipo mikononi mwako.

Mbali na uozo huo ni udhalilishajwi wa wanawake kwani kuna kipindi baadhi yao wanajifungua wodini hapo sehemu za wazi bila hata ya kuzungushiwa mapazia ambapo wanawake wenzao huwashuhudia.

Kama hiyo haitoshi hata wanaume ambao wanapita nje au wengine wanakuja pale kwa ajili ya kuwajulia hali ndugu zao wanawaona wakinamama hao kwakuwa madirisha yapo wazi.

Waziri Mwakyusa utatufurahisha Watanzania utakapochukua hatua za kinidhamu kwa wahusika hospitialini hapo, tena si Amana tu bali kuna hosptitali nyingi za serikali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kila kukicha na matokeo yake viongozi wake wamekuwa wakikanunsha madai hayo na kufanya wanahabari tuonekane tunaandika wanaandika uongo.

NB: MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA NINALOFANYIA KAZI

Comments

  1. Dada Dina pole sana na msukosuko uliokukuta kwani hao si wauuguzi bali ni wauwaji hizi habari ulizotoa mimi naamini kabisa kwani nishawahi kuzisikia hapo Amana wakati mke wangu alipojifungua mtoto wangu wa2 1992 tena wakati huo walikuwa wanakuambia uende na pamba na mkasi pamoja na shilingi 5000 za muuguzi atakae kushughulikia. kweli kabisa huyo waziri wa wizara hiyo anatakiwa afanye kweli kukomesha uzalimu huo.
    Wako
    mdau james
    Holland

    ReplyDelete

Post a Comment